Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania

To protect the rights of content creators...
COSOTA KUSHIRIKIANA NA NBS  KUFANYA UTAFITI WA KUHUISHA TAARIFA YA MWAKA 2012 YA MCHANGO WA HAKIMILIKI KATIKA PATO LA TAIFA 
05 Dec, 2023
COSOTA KUSHIRIKIANA NA NBS  KUFANYA UTAFITI WA KUHUISHA TAARIFA YA MWAKA 2012 YA MCHANGO WA HAKIMILIKI KATIKA PATO LA TAIFA 


Ofisi ya Hakimiliki Tanzania - COSOTA yafanya mazungumzo na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuhusu kushirikiana katika kufanya utafiti wa kuhuisha taarifa ya mwaka 2012 ili kuangalia namna hakimiliki inavyochangia katika pato la taifa.

Kikao hicho kimefanyika leo Disemba 05, 2023 baina ya Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki wa COSOTA Bi. Doreen Anthony Sinare na Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Jijini Dodoma pamoja na timu ya wataalamu kutoka COSOTA, NBS na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Akizungumza katika kikao hicho Afisa Mtendaji Mkuu  wa COSOTA alieleza kuwa Shirika la Miliki Bunifu Duniani kwa kushirikiana na COSOTA na BRELA walifanya utafiti huo nchini Tanzania kwa taarifa ya jinsi Hakimiliki ilivyochangia katika pato la taifa mwaka 2009 - 2010 na ripoti yake  ilitoka mwaka 2012.

"Tukiangalia ripoti hii ya utafiti ni ya muda mrefu na mambo mengi yamebadilika hivi sasa, nimewasiliana na WIPO kwa ajili ya kushirikiana nao katika kufanya utafiti huu na wameridhia kutoa ushirikiano. Hivyo kwa sasa Lengo ni tuandae timu ya Wataalamu wa Takwimu, Uchumi na Hakimiliki na kuweka mkakati wa namna ya kutimiza Lengo hilo. Utafiti huu pia utapelekea utolewaji wa tuzo kwa wale waliochangia zaidi katika pato la taifa na itajenga uelewa na kutoa picha halisi ya umuhimu wa hakimiliki katika Taifa," alisema Doreen.

Kwa upande wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt.Albina Chuwa (NBS) alisema Ofisi ya Takwimu itatoa ushirikiano katika kufanikisha utafiti huo na kuwa utafiti huu ni muhimu sana.

"Suala la kuandaa mpango wa utekelezaji wa utafiti huu ufanyike Kwa haraka na Maafisa waliopewa jukumu hili mtoe kipaumbele n kujito katika kazi hii ili kuleta tija iliyokusudiwa bila kuchelewa" alisema Dkt.Albina.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uchumi na Takwimu Bw. Daniel Msolwa alipongeza COSOTA kwa jitihada za kufikiria kuhuisha utafiti huo, na kusema kweli kuna umuhimu mkubwa wakufanya utafiti huo sababu kwa sasa kuna changamoto ya taarifa za eneo hilo kukosekana.

"Ni vyema kwa sasa tuweke mkakati wa namna ya kufanya hii kazi na kujua kuhusu upatikanaji wa rasilimali za kufanya kazi hii sababu ni kazi kubwa na tunaamini WIPO pamoja na Shirika la Kikanda la Afrika la (ARIPO) watasaidia katika kufanikisha suala  hili,"alisema Msolwa.

Pamoja na hayo Doreen alishukuru utayari wa NBS na BRELA ambaye ndio Msimamizi Mkuu wa Miliki Bunifu Tanzania (Intellectual Property Office) kushirikiana na COSOTA.