Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania

To protect the rights of content creators...
WANAWAKE WABUNIFU WASISITIZWA KURASIMISHA KAZI ZAO
05 May, 2023
WANAWAKE  WABUNIFU WASISITIZWA KURASIMISHA KAZI ZAO

Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki kutoka Ofisi ya Hakimiliki Tanzania - COSOTA Doreen Anthony Sinare atoa wito kwa Wabunifu Wanawake nchini kuhakikisha wanarasimisha kazi zao za ubunifu ili kuweza kunufaika zaidi.

Doreen ametoa wito huo leo Aprili 26, 2023 katika mkutano wake na wabunifu wanawake uliyojukikana kama "CUP OF TEA WITH COSOTA CEO" ambao ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku Miliki Bunifu Duniani ambayo hufanyika kila tarehe 26 Aprili Kimataifa  na huratibiwa na Shirika la Kimataifa la Miliki Bunifu Duniani (WIPO).

"Maadhimisho ya mwaka huu wa 2023 katika Siku ya Miliki Bunifu Duniani yamelenga zaidi kuhamasisha wanawake wanaofanya shughuli za ubunifu kuongeza juhudi katika kazi zao na kuzirasimisha ili waweze kunufaika zaidi na kauli mbiu yake ni 'Wanawake na Miliki bunifu kuchochea ubunifu', hili ni fursa kwa wanawake hivyo tuitumie vizuri,"alisema Doreen.

Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo Afisa Mtendaji Mkuu huyo na Msimamizi wa Hakimiliki nchini aliwasisitiza wanawake hao kutokubali kukatishwa tamaa kwa jambo lolote ambalo wanahitaji kufanya na pale wanapohitaji ushauri yupo tayari kuwasaidia, au wanaweza kufika Ofisi za COSOTA kuomba ushauri.

Naye Wakili wa Wasanii Annamaria Ishengoma kutoka Ofisi ya Mawakili Quinn alitoa ushauri wa jinsi ya kulinda bidhaa za "fashion" na  kusisitiza masuala ya usajili wa kila kitu kwa kuhakikisha kama Jina la Kampuni na bidhaa nayo inapewa jina na  kulisajili.

Pamoja na hayo Wanawake hao wabunifu walipata fursa ya kuzungumzia mazingira ya shughuli zao na changamoto wanazokutana nazo na mambo waliyoweza kuwafanya wakate taama, ambapo walipata ufafanuzi na ushauri kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki ambapo aliwasisitiza kusajili kazi zao na kuhakikisha wanarasimisha na kupata ushauri mara kwa mara bila kukubali kukatishwa tamaa kama mmoja ya wadau alipoonesha kukata tamaa kutokana na kukosa uelewa wa masuala ya miliki ubunifu. Walisitizwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu kutoka COSOTA na BRELA na kuwa makini katika mikataba wanayosaini kibiashara na wadau mbalimbali.