Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania

To protect the rights of content creators...
WAZIRI BALOZI DKT.PINDI CHANA AIPONGEZA COSOTA KWA KUKAMILISHA KANUNI YA MAREKEBISHO YA SHERIA YA MWAKA 2022
17 Apr, 2023
WAZIRI BALOZI DKT.PINDI CHANA AIPONGEZA COSOTA KWA KUKAMILISHA KANUNI YA MAREKEBISHO YA SHERIA YA MWAKA 2022

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Balozi Dkt.Pindi Chana ameipongeza Ofisi ya Hakimiliki kwa utendaji na kwa maboresho mbalimbali ya kiutendaji katika mabadiliko ya sheria na uundwaji wa Kanuni mbalimbali.

Mheshimiwa Waziri  Balozi Dkt.Chana ametoa pongezi hizo katika ziara yake ya kwanza (mara baada ya kuapishwa) katika Ofisi hiyo iliyolenga kufahamu majukumu ya taasisi zilizochini ya wizara hiyo.

"Bado mnajukumu kubwa la kuendelea kusimamia kazi za wasanii na waandishi katika aina zote ili wanufaike zaidi" alisema Mhe.Balozi Dkt.Chana.

Pamoja na hayo Waziri huyo alitoa maelekezo kwa COSOTA kukaa pamoja na BASATA na Bodi ya Filamu kuona namna gani suala la makusanyo linaweza kuratibiwa kwa urahisi bila kuwa kero kwa wafanyabiashara na kuweza kuishauri Wizara ili kupunguza changamoto ya mdau mmoja kudaiwa na Ofisi tatu zenye kutumia kazi za Sanaa.

Vile vile ameielekeza COSOTA kuendelea kutoa elimu ya hakimiliki na njia ya makongamano na semina kabla ya kuanzishwa kwa Kampuni za kukusanya na kugawa Mirabaha.

Aidha, nae Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo alisisitiza COSOTA kuendelea kufanya jitihada za kupatikana kwa mfumo wa ufuatiliaji wa matumizi ya kazi zinazolindwa na hakimiliki kama Muziki na Filamu pamoja na kugawa Mirabaha ili kuhakikisha kuwa  Makampuni hayo yatakapoanzishwa  yanakuwa na mfumo huo.

Halikadhalika nae Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Doreen Anthony Sinare aliiomba Wizara kuisaidia COSOTA kupata fedha kwa ajili ya kuweza kupata mfumo huo kupitia bajeti ya Serikali.