COSOTA YAGUSA MAISHA YA WAGONJWA TAASISI YA SARATANI OCEAN ROAD KUELEKEA MEI MOSI 2026
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani tarehe 1 Mei 2026, Wafanyakazi wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) leo tarehe 30 Aprili, 2026 wamefanya ziara ya kutembelea Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa lengo la kuwafariji wagonjwa na kuchangia sehemu ya gharama za matibabu kama matendo ya huruma kwa wagonjwa wanaopata matibabu hospitalini hapo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Taasisi (COSOTA) Bi. Asela Mathew Mwaiswelo ameeleza kuwa uamuzi wa kutembelea Taasisi hiyo umechochewa na utamaduni wa kurudisha fadhila kwa jamii na kutambua kuwa wagonjwa wengi ni sehemu ya nguvu kazi ya Taifa inayohitaji faraja ili kurejea katika ujenzi wa Taifa!
Naye Meneja wa Huduma za Ustawi wa Jamii Bw. Malkiory Niniko (wa nne kulia) na Afisa Ustawi wa Jamii Bi. Karafuu Yusuphy (wa sita kushoto) pamoja na uongozi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road wameishukuru COSOTA kwa moyo huo wa upendo, wakieleza kuwa kitendo hicho kinasaidia kuongeza hali ya matumaini kwa wagonjwa na kupunguza baadhi ya changamoto ya mahitaji ya kila siku.
Maadhimisho ya Mei Mosi 2026 yamebeba kauli mbiu inayosisitiza “Kazi zenye Staha kwa Maendeleo endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050” mambo ambayo COSOTA imeamua kuyaishi kwa kuwajali wale ambao kwa sasa wapo nje ya mazingira ya kazi kutokana na changamoto za kiafya
