SERIKALI KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUPAMBANA NA UHARAMIA
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Ndg. Gerson Msigwa atoa wito kwa Watanzania kuungana pamoja kupambana na uharamia wa kazi za Sanaa ili Wasanii na wawekezaji wa Sekta ya kazi za Sanaa na Michezo waweze kuendelea kusaidia katika ukuaji wa sekta hiyo.
Ndg. Msigwa ametoa wito huo Mei 18 2026 alipokuwa akifungua Kongamano la majadiliano ya namna ya kupambana na uharamia wa kidijitali (digital piracy).
"Sekta ya Habari, Sanaa na Michezo zinakuwa kwa kasi, ukuaji huu unapaswa kuzingatia msingi wa hakimiliki na kazi zake kulindwa kisheria ili Wabunifu na wawekezaji waweze kunufaika na niwaahidi yale yote mtakayokubaliana katika kongamano hili Serikali tupo tayari kupokea maoni yenu na kuwapa ushirikiano," alisema Ndg. Msigwa.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) Bi. Naomi Mungure alisema mkutano huo umehusisha wadau mbalimbali ikiwemo Taasisi za Serikali, Wasanii, Mahakama, Jeshi la Polisi, Sekta binafsi ikiwemo watoa huduma za mitandao, Wazalishaji na Wasambazaji kazi za Sanaa na Michezo pamoja na Wamiliki wa Vyombo vya habari.
Akiendelea kuzungumza Bi. Naomi alisema lengo la Kongamano hilo ni kupata maoni na kuunda mkakati wa pamoja wa namna bora ya kupambana na uharamia wa kidijitali.
Pamoja na hayo akizungumza katika mkutano huo Mtaalam wa mbinu za teknolojia za kudhibiti miundombinu ya uharamia kidijitali Bw. Levacher Antoine Clement alieleza kuwa udhibiti wa uharamia katika mitandao unaweza kufanyika.
