COSOTA YAIPONGEZA TAVIC
Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) yaipongeza Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ya Tanzania Audiovisual Collection (TAVIC) inayokusanya mirabaha katika kazi za daraja la vielelezo vya kusikia na kuona ) kwa mkakati wa kuunda timu ya Mawalaka wa kukusanya mirabaha katika Kanda tano nchini .
Pongezi hizo zimetolewa na Maafisa wa COSOTA waliyotembelea Kampuni hiyo Septemba 30, 2026 jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupata taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu pamoja na changamoto ikiwa ni sehemu ya majukumu ya COSOTA katika usimamizi.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Uendeshaji Bi. Anna Roman alisema ukusanyaji wa mirabaha katika kanda tano utaanza mwezi Oktoba 2026, kwa Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Pwani na Kanda ya Mashariki na viongozi wa kanda hizo wamepewa malengo katika kutimiza jukumu la ukusanyaji.
Pamoja na hayo katika kikao hicho TAVIC waliwasilisha taarifa mbalimbali ikiwemo hatua za makusanyo ya mirabaha, usajili wa wanachana na mpango wa kampuni hiyo katika kujitangaza ili kuweza kufikia wadau wengi pamoja na kufahamu changamoto wanazopitia ili COSOTA iweze kuwasaidia.
Hata hivyo COSOTA ilitoa maelekezo kwa kampuni hiyo kuongeza bidii kujitangaza kwa njia mbalimbali ikiwemo kwa kutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ili wadau waweze kuwafahamu, pia COSOTA ilisisitiza kuwa wanaweza kushirikiana nao katika kujitangaza na wapopata changamoto katika utekelezaji wa majukumu wanaweza kutoa taarifa ili kupata usaidizi.
Halikadhalika Kampuni ya TAVIC inakusanya mirabaha katika maeneo ya Hoteli, Kumbi za Starehe, Vyombo vya Usafiri, Benki n.k. na Maafisa walioshiriki katika kikao hicho ni Bw. Prosper Massawe kutoka Kitengo cha Uzingatiaji, Bi. Rhoda Lupondo kutoka Kitengo cha Leseni na Uharamia pamoja na Bi. Anitha Jonas Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano.
