COSOTA YATUMIA JUKWAA LA CISAC KUIMARISHA MASUALA YA HAKIMILIKI AFRIKA
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, leo amekutana na ujumbe wa Tanzania kutoka Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) uliohudhuria mkutano wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Watunzi na Wasanii (CISAC Regional Committee for Africa - CAF) uliofanyika tarehe 1 na 2 Juni 2026 mjini Paris, Ufaransa.
Ujumbe huo uliongozwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki wa COSOTA, Bi. Naomi Mungure, na ulijumuisha aliyekuwa Afisa Sheria Mwandamizi wa COSOTA, Bi. Maureen Fondo ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Hakimiliki katika Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (ARIPO), pamoja na aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki wa COSOTA, Bi. Doreen Sinare.
Katika mazungumzo hayo, ujumbe ulimweleza Balozi kuhusu mijadala iliyofanyika katika mkutano huo ikiwemo maendeleo, fursa na changamoto zinazotokana na matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence) katika sekta ya hakimiliki, mifumo ya usajili na uhakiki wa kazi za ubunifu, ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha, tozo za hakimiliki (Private Copy Levy), haki za wasanii kupata mapato kutokana na mauzo ya kazi zao katika minada (Resale Rights), pamoja na umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za hakimiliki barani Afrika.
Aidha, Balozi Yakubu alipata fursa ya kufahamu shughuli za kitaaluma zinazoendelea kufanywa na wataalamu hao wa Kitanzania ambapo Bi. Maureen Fondo anaendelea na utafiti wa Shahada ya Uzamivu (PhD) unaohusu utekelezaji wa hakimiliki katika kazi za sanaa za ufundi zinazozalishwa kwa kutumia Akili Unde nchini Tanzania, wakati Bi. Doreen Sinare anafanya utafiti kuhusu namna ya kuimarisha ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya hakimiliki katika sekta ya muziki barani Afrika.
Balozi Yakubu aliwapongeza wajumbe hao kwa kuiwakilisha Tanzania vyema katika jukwaa hilo muhimu la kimataifa na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya hakimiliki nchini ili kulinda ubunifu, kuongeza mapato ya wasanii na kuchochea ukuaji wa uchumi wa ubunifu unaoendelea kupewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita.
