MHE. MWINJUMA AWAGEUKIA MAHARAMIA WA KAZI ZA MAANDISHI
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, ameitaka Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kushirikiana kwa karibu na Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA) katika kuwasilisha taarifa za operesheni na kesi zilizofunguliwa dhidi ya maharamia wa kazi za maandishi pamoja na kuandaa mpango kazi wa namna ya kupambana na Uharamia wa kazi za maandishi.
Mhe. Mwinjuma ameyasema hayo Oktoba 12, 2026, wakati akifungua rasmi Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania yaliyofanyika katika Viwanja vya Maktaba ya Taifa jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mwinjuma amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya uharamia wa vitabu lazima yapewe kipaumbele ili kulinda haki na maslahi ya waandishi na wachapishaji nchini.
"Tuna kikao na COSOTA na najua katika ajenda zetu hili suala hatukuliweka, ila naomba liwekwe kwenye ajenda tutakazojadili kwenye kikao chetu cha hivi karibuni," amesema Mhe. Mwinjuma.
Aidha Mhe. Mwinjuma ameeleza kuwa vitabu si nyenzo tu za kujifunzia darasani, bali ni hazina ya kumbukumbu za taifa, daraja linalounganisha vizazi, na njia kuu ya kukuza fikra, ubunifu pamoja na uwezo wa jamii kujielewa.
"Historia ya taifa lolote haiwezi kuhifadhiwa na kurithishwa kwa ukamilifu bila maandishi, machapisho na taasisi zinazoyatunza. Kwa sababu hiyo, kuendeleza utamaduni wa kusoma, kuandika na kutunza vitabu ni sehemu muhimu ya kuendeleza taifa letu," aliongeza.
